Azam, Yanga kazi haijaisha Afrika.


Katuni.
Mwishoni mwa wiki timu za Azam na Yanga zilifanya vizuri katika mechi za kimataifa ugenini huku JKU ya Ligi Kuu ya Zanzibar ikikumbana na kipigo jijini Kampala, Uganda.
 
Yanga iliyokuwa ugenini kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, Rwanda, iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji APR FC katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
 
Azam FC walichomoza na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Bidvest Wits mjini Johannesbrug, Afrika Kusini katika mechi yao ya kwanza ya Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho.
 
Wawakilishi pekee wa Zanzibar waliosalia kwenye michuano ya Afrika mwaka huu, JKU FC wakitandikwa magoli 4-0 dhidi ya SC Villa ya Ligi Kuu ya Uganda na kufifisha ndoto zao za kutinga Raundi ya Pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
 
Timu hizo zitarudiana Tanzania mwishoni mwa wiki hii, Yanga wakiwakaribisha APR kwenye Uwanja wa Taifa, wakati Azam FC watakuwa katika maskani yao yaliyopo Chamazi, huku JKU wakishuka kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
 
Tukiwa wadau namna moja wa michezo nchini, Nipashe tunawapongeza Azam FC na Yanga kwa kupambana na kupata ushindi ugenini licha ya kucheza dhidi ya timu zenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa.
 
Mara nyingi viwanja vya ugenini vimekuwa vikionekana changamoto kubwa kwa mafanikio ya timu za Tanzania ambazo zimekuwa zikitolewa hatua za awali katika michuano ya kimataifa. Pengine msimu huu ni mzuri kwa Wanalambalamba na Wanajangwani. 
 
Rekodi ya juu kwa timu za Tanzania katika mashindano ya Afrika ilikuwa 2003 Simba ilipotinga hatua na makundi na hatua kama hiyo kufikiwa na Yanga mwaka 1998. Simba pia iliingia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka 1993.
 
Ushindi wa Azam na Yanga katika mechi za juzi umeonyesha njia ya mafanikio kwa klabu za soka za Tanzania kimataifa, Lakini unahitaji kulindwa nyumbani mwishoni mwa wiki. 
 
Tunaamini ushindi huo wa ugenini si sababu kuntu kwa timu hizo kubweteka na kuona tayari zimeshafuzu kutinga Raundi ya Pili kutokana na ukweli kwamba wapinzani wao wanao uwezo wa kushinda ugenini.
 
Kutokana na ukweli huo, tunatoa rai kwa klabu za Azam na Yanga na hata JKU kujipanga zaidi kwa mechi za marudiano kuhakikisha wanashinda mechi za mwishoni mwa wiki dhidi ya wapinzani wao.
 
Tunafahamu kila timu imejiandaa, lakini siku zote tunaamini kuwa, timu inayojiandaa kushinda nyumbani na ugenini ndiyo inayokuwa jirani na mafanikio katika mashindano ya mtindo wa mtoano kuliko ile isiyofanya hivyo.
 
Ndiyo maana tunasema Azam na Yanga bado hawajamaliza kazi Afrika licha ya kupata ushindi katika mechi zao za ugenini Rwanda na Afrika Kusini.
 
Tunaamini mipango mizuri ya mechi zao za marudiano, itakuwa sehemu ya maandalizi yao ya mechi za hatua inayofuata ya Raundi ya Pili ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho, ikizingatiwa kuwa watakutana na timu kubwa. Yanga, kwa mfano, wakiing'oa APR, watacheza dhidi ya Al Ahly ambayo iliwang'oa mwaka juzi.