Hongera Dk. Shein, lakini Zanzibar inahitaji umoja.


Katuni.
Juzi Zanzibar ilifanya uchaguzi wa marudio wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani, ambao ulimpa ushindi wa asilimia 91.4 mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein.
 
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, kwa madai kuwa ulijaa kasoro kadhaa.
 
Hata hivyo, uamuzi wa Jecha ulikosolewa na makundi kadhaa wakiwamo waangalizi wa kimataifa wakisema katika ripoti yao ya awali kuwa ulikuwa mzuri kuliko hata wa mwaka 2010.
 
Chama cha wananchi (CUF) ambacho ni chama kikuu cha upinzani Zanzibar kilipinga maamuzi ya Jecha na kutangaza kutoshiriki katika uchaguzi wa marudio kwa kuwa kinatambua uchaguzi halali ni uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
 
Kimsingi, kumekuwapo na mgawanyiko miongoni mwa Wazanzibari baada ya tangazo la Jecha la kufuta matokeo hayo na kutangaza uchaguzi wa marudio. Mgawanyiko huo umejikita zaidi katika itikadi za vyama vya CCM na CUF.
 
Tunachukua fursa hii kumpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata na ni matumaini yetu kwamba atahakikisha kwamba anafanya kila liwezekanalo kuinua uchumi wa Zanzibar sambamba na kuwapatia Wazanzibari wote maendeleo.
 
Tunaamini kwamba hilo atalitekeleza kwa kuwa jana wakati akitoa shukrani baada ya kutangazwa mshindi na kukabidhiwa cheti cha ushindi na Jecha, alisema Zanzibar itatumia kila rasilimali iliyopo kuhakikisha inajitegemea.
 
Hata hivyo, ni jambo lililo wazi kwamba Wazanzibari wamegawanyika tena kutokana na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana na ndiyo maana CUF yenye wafuasi wengi hususani Pemba haikushiriki katika uchaguzi wa juzi.
 
Kutoshiriki kwa CUF ni dhahiri kuwa Wanzanzibari wanaokiunga mkono chama hicho watakosa uwakilishi katika vyombo muhimu vya maamuzi kwa maana ya Baraza la Uwakilishi na mabaraza ya madiwani.
 
Baada ya kupatikana maridhiano mwaka 2010 na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyovishirikisha CCM na CUF, Zanzibar ilipata ululivu wa kisiasa na kumaliza uhasama uliokuwapo tangu kabla  ya Mapinduzi ya Zanzibar na ulioendelea baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
 
Ushindi alioupata Dk. Shein na wagombea wa uwakilishi wa CCM umeifuta SUK na hata kama itaundwa, haitakuwa na maana yoyote kwa kuwa ukweli uko dhahiri kwamba serikali hiyo inaundwa kutokana na kuwapo na CUF na siyo vyama vingine ambavyo havina wafuasi visiwani humo na ndiyo maana hauina kilichopata asilimia 10.
 
Itakumbukwa kuwa kila uchaguzi tangu mwaka 1992 hadi 2010 CCM na CUF vimekuwa vinatofautiana kwa idadi ndogo ya kura, hali iliyokuwa inaonyesha kwamba hakuna chama cha kuunda serikali peke yake.
 
Kwa kuwa uchaguzi umefanyika kwa kufuata Katiba ya Zanzibar, hakuna sababu ya kupinga matokeo yake, lakini ni lazima jitihada zikafanyika ili kumaliza mgawanyiko uliopo kwani uchaguzi huo sio mwarobaini wa mpasuko wa kisiasa unaoikabili Zanzibar.
 
Njia pekee ni meza ya mazungumzo ambayo itavishirikisha CCM na CUF ambavyo vina wafuasi. Tunawaomba wale wote wanaojali maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Bila Zanzibar yenye umoja, itakuwa vigumu kuwapo maendeleo.
SOURCE: NIPASHE