Michuno hii mikubwa ya kimataifa, hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne na kushirikisha mataifa mbalimbali duniani.
Zaidi ya michezo 50, ukiwamo soka hushindaniwa kwenye mashindano haya ya pekee na aina yake.
Tanzania ni moja ya nchi zinazotarajia kupeleka wawakilishi watakaoshindana katika michezo hiyo.
Ingawa kuna michezo zaidi ya 50 inayoshindaniwa, Tanzania itapeleka wawakilishi katika michezo mitatu; Judo, riadha na kuogelea.
Hata hivyo, pamoja na Tanzania kutuma wawakilishi kwenye mashindano haya kila yanapofanyika, bado hakuna mafanikio ya kujivunia.
Sababu kubwa ambayo imekuwa kama wimbo kwa Tanzania kushindwa kupata mafanikio ni maandalizi duni.
Maandalizi ya zima moto kwa wanamichezo wetu katika mashindano mbalimbali, ndiyo kiini cha kushindwa kufanikiwa.
Kwa wenzetu wanaopenda mafanikio na ndiyo ambao leo wanaendelea kufanya makubwa katika mashindano ya kimataifa, hujiandaa mara tu mashindano ya awali yanapomalizika.
Hawana muda wa kusubiri hadi mashindano yanapokaribia ndipo waanze maandalizi kama tunavyofanya sisi.
Katika hali ya maandalizi ya aina hii, hatuwezi kupata mafanikio. Pengine sifa kubwa itakuwa ni ushiriki usio na tija.
Sisi kama wapenda michezo, tulitarajia kuona vyama vinavyojiandaa kupeleka wawakilishi kuanza maandalizi mapema zaidi kwa sababu inafahamika kila baada ya miaka minne mashindano yanafanyika.
Leo hii tunaweka kambi kuwa msingi pekee wa kufanya vizuri, wakati maandalizi yalitakiwa kuanza tangu mashindano ya miaka minne iliyopita yalipomalizika.
Kwa mashindano yanayofanyika kila baada ya miaka minne, hatuwezi kujiandaa katika utamaduni wa ‘zima moto’ na bado tukatarajia kurejea na medali.
Udhaifu wa viongozi wa vyama husika katika kupanga, kusimamia na kutekeleza mahitaji ya maandalizi kabla ya kushiriki mashindano ndiyo mambo yanayoikwamisha Tanzania kufanya vizuri kwenye mashindano.
Viongozi hawana ubunifu ndiyo maana kila kukicha hawaishi kulalamika suala la ukata. Leo Tanzania haitapeleka wawakilishi wa mchezo wa ngumi na sababu kubwa ni kukosa fedha za kuwapeleka mabondia kwenye mashindano ya kufuzu.
Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 45, ina wanariadha wawili tu waliofuzu kwa michezo hiyo mwaka huu kwa mbio za marathoni.
Michezo mingine kama Judo na Kuogelea bado hakuna mwanamichezo aliyefuzu na huenda tukashindwa kupeleka wawakilishi kama watashindwa kufikia viwango.
Tuwe wakweli, kama tuna dhamira ya kuiondoa Tanzania katika usingizi, lazima tuje na mikakati mizuri ya kuwaandaa wanamichezo mapema.
Tanzania ya sasa inahitaji viongozi wabunifu na wasiotumia muda mwingi kulalamika kuhusu ukata, bali watakaotumia nafasi zao kutafuta vyanzo mbalimbali vya fedha kuwaandaa wanamichezo wao.
SOURCE: THE GUARDIAN