Yanga wajipange kufuta uteja Al Ahly


Katuni.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanznia Bara, timu ya Yanga wamefanikiwa kutinga raundi ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya juzi kuing'oa klabu ya APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
Wanajangwani walishinda 2-1 ugenini jijini Kigali wiki mbili zilizopita kabla ya juzi kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya timu hiyo ya Jeshi la Rwanda.
 
Kabla ya kuivaa APR, Yanga iliikabili Cercle de Joachim ya Mauritius na kuitua nje ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu barani kwa jumla ya mabao 3-0.
 
Kwa kutinga raundi ya pili, Yanga sasa itakuwa na kazi ngumu itakapochuana na Al Ahly ya Misri kwa mara nyingine baada ya msimu mmoja.
Timu hiyo ya Ligi Kuu ya Misri iliing'oa Yanga katika michuano ya Afrika mwaka juzi katika hatua ya matuta baada ya kutoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida, kila timu ikishinda nyumbani.
 
Takwimu za soka zinaonyesha timu za Tanzania zimekuwa zikitolewa mara nyingi kwenye michuano ya Afrika na timu za kaskazini mwa Afrika (za Kiarabu). Kutokana na ukweli huo, Nipashe tunaona kuna haja Yanga kufanya maandalizi ya kina kabla ya kuwavaa Al Ahly.
 
Timu za Kiarabu zinasifika kwa kuwa na mipango mizuri ya nje na ndani ya uwanja katika kusaka matokeo. Yanga wanapaswa kujipanga kikamilifu kuhakikisha wanadhibiti mianya ya fitna za Al Ahly.
 
Na kama kweli wamedhamiria kulipa kisasi cha matokeo mabaya ya mwaka juzi, tunafikikri Yanga wanapaswa kuanza maandalizi mapema kabla ya kukutana nao.
 
Licha ya kufanya vizuri katika raundi mbili zilizopita, tunaamini kikosi cha Yanga kinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zisizofanyiwa kazi mapema, zitakuwa na athari kubwa mbele ya nyota wa Al Ahly wasiofanya makosa mengi wanapokuwa na nafasi ya kuifunga timu pinzani.
 
Katika mechi mbili zilizopita dhidi ya APR, kwa mfano, Yanga imeruhusu mabao mawili na safu zake zote kuanzia ulinzi hadi ushambuliaji zilionekana kuyumba.
 
Tunafahamu kuna changamoto ya kuwa na majeruhi kadhaa kikosini, lakini Yanga ilisajili nyota 24 kwa ajili ya msimu huu ambao tunaamini wakielezwa mbinu chafu na fitna za timu za Kiarabu, wanaweza kutinga robo-fainali kwa kuing'oa Al Ahly na kuiwakilisha vyema Tanzania msimu huu.
 
Al Ahly iliyoanzishwa Aprili 24, 1907 (miaka 28 kabla ya Yanga kuanzishwa), ina rekodi nzuri katika mashindano ya Afrika, Timu hiyo imeshinda mataji nane ya Ligi ya Mabingwa na moja la michuano ya Kombe la Shirikisho.
 
Tunafahamu pia kuwa Al-Ahly ndiyo timu namba moja duniani kwa kushinda mataji mengi ya kimataifa (Klabu Bingwa duniani) wakifanya hivyo mara 20 na kuzipiku AC Milan, Real Madrid na Boca Juniors.
 
Lakini mpira unadunda, Yanga walikaribia kuing'oa mwaka juzi, tunaamini wanaweza kupata mafanikio hayo mwaka huu.
 
Ndiyo maana tunatoa rai kwa uongozi wa Yanga na benchi lao la ufundi kujipanga vyema ili kupata matokeo mazuri nje-ndani dhidi ya timu hiyo
 
SOURCE: NIPASHE